Ukristu ni Furaha

NI UFALME WA FURAHA

Jumapili ya 28 ya Mwaka A

 

Waheshimiwa wapendwa,

Leo tunakumbushwa kuwa Ufalme wa Mungu ni Ufalme wa Furaha; lakini mara nyingi tunapoalikwa katika ufalme huo tunakataa mwaliko; tunahangaikia shughuli zetu za maisha ya hapa duniani na kushindwa kushughulikiwa maisha katika ufalme wa Mungu. Matokeo yake ni kukosa hizo furaha. Tumwombe Mungu atufungue macho ya mioyo yetu ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo ili shughuli za duniani zisitusahaulishe Ufalme wa Mungu.

Kutokana na masomo ya leo tujifunze yafuatayo:

1. Ukristu ni furaha

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anaagua nyakati za furaha ambapo Bwana atawaandalia karamu watu wake na kufuta machozi katika nyuso zote.

Katika Enjili Kristu anaonyesha kuwa nyakati hizo zimetimilika kwa kuja kwake. Bwana tayari ameandaa karamu na anataka kufuta machozi kutoka nyuso za watu. Lakini cha kushangaza walioalikwa kwenye karamu wanakataa mwaliko huo. “Alikuja kwa walio wake lakini walio wake hawakumpokea” (Yn 1:11)

Karamu hii ni mfano wa Ufalme wa Mungu. Tunapoitwa katika Ufalme wa Mungu kwa njia ya Ukristu inapaswa kuleta furaha katika maisha yetu. Ukristu ni furaha.

Kwa nini Ukristu ni furaha? Ni nini kilatea furaha katika Ukristu?

a)      Tunakuwa watoto wa Mungu

Yohane anatwambia “Lakini wale wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu” (Yn 1:12).

Faida za kuwa watoto wa Mungu

  • Tunakuwa na haki ya kifamilia katika familia ya Mungu.

Basi ninyi si wageni tena, wala si watu wan je. Nyinyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu jamaa ya Mungu”  (Efe 2:19)”

  • Tunaweza kumwita Mungu “Baba.”  “Kwa vile sasa ninyi ni wanawe, Mungu amemtuma Roho wa Mwanae mioyoni mwenu, Roho aliaye ‘Aba’ yaani ‘Baba’” (Gal 4:6).
  • Tunaweza kuhusiana na Mungu na kumuomba mahitaji yetu kama wana si kama watumwa. “Basi, wewe ni mtumwa tena, bali mwana. Na ikiwa ni mwana, basi, wewe utapokea yote Mungu aliyowawekea watoto wake”(Gal 4: 7).

Kwa hiyo tunakuwa na maisha yenye uhakika na furaha;  hata katika mateso tunajua kuwa tunaye Baba abayetujali; tukitenda dhambi tunajua kuwa atatuhurumia na kutusamehe.

Mara nyingi tunahesabu faida za Ukristu katika mali za kidunia; tusipopata pesa basi ukristu hauna maana. Hata wengine huogopa kujihusisha sana na maswala ya kanisa kwa fikra kuwa watakuwa maskini. Tatizo ni kutojua kipi kilatea furaha. Ndiyo maana tunamuomba Mungu atufungue macho ya mioyo yetu ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.

 

b)      Tunajua mapenzi ya Mungu

Furaha ni hali ya kuridhika inayoletwa na tendo jema. Tendo jema ni lile linaloendana na mapenzi au amri za Mungu. Ukristu unatufundisha mapenzi ya Mungu. Hivyo, Ukristu unaleta furaha. Mara nyingi tunalalamikia amri za Mungu na miongozo ya Kanisa kwamba inatunyima uhuru. Lakini ukweli ni kwamba amri za Mungu ndizo zinatusaidia kujua na kutenda lililojema na hivyo kuwa huru “Ukweli utawaweka huru” na furaha.

 

c)       Kristu anatufundisha maana mpya ya mateso

Tunaweza kujiuliza: Kama kweli Ukristu ni furaha na Mungu ameahidi kufuta machozi kutoka nyuso zetu, mbona bado tunaendelea kulia kwa sababu ya matatizo na ugumu wa maisha?

Matatizo tunayokumbana nayo maishani yana sababu nyingi (rej Makala: How to handle suffering by Fr Achilles). Ukristu hautaondoa matatizo ya maisha lakini utatupatia mbinu za kukabiliana na matatizo hayo; utatupatia maana na faida ya mateso hayo – huwezi kuona maana ya mateso isipokuwa kwa macho ya imani.

 

Ndiyo maana Pauo anatwambia katika somo la piliNajua kudhilika, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.

 

Lakini ni kitu gani kinampatia uwezo huo? Paulo anasemaNayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.

Kristu ambaye alikuwa yu namna ya Mungu lakini akaachilia hayo yote akawa mtii hata mauiti naam mauti ya msalaba (rej Wafil 2:6ff) huyo ndiye anayenitia nguvu katika mateso kwa sababu yeye hakuishia msalabani au kaburini. Hii ndiyo initiayo nguvu kwa sababu “tunajua kuwa yule aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi pia pamoja na Yesu” (2Kor 4:14).

Kwa hiyo hata nikiwa katika matatizo ya namna gani maishani: iwe ugumu wa maisha, iwe kuteseka kwa imani yangu, iwe kunyanyaswa na wengine, iwe ni kudhulumiwa kwa sababu ya uongozi au msimamo wangu katika imani na maadili,  ninapata kitulizo kwambaBaada ya dhiki kuna faraja” na “Mchumia juani hulia kivulini.”

Kwa hiyo tunakuwa na furaha hata katika mateso. Ukristu ni furaha. Unatuwezeka kuseme kama Paulo kuwa

Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristu kwa ajili ya mwili wake yaani Kanisa ”(Kol 1:24).

Kama tulivyodokeza kuwa mateso yana sababu nyingi; hapa tunazungumzia mateso kwa ajili ya kutenda mema kama Petro anavyotuonya:

 “Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema kama Mungu amependa hivyo, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu”(1Pet 3:17).

d)      Tunaahidiwa uzima wa milele

Sherehe za Ufalme wa Mungu tayari zinapaswa kuanza hapa duniani lakini zitakamilika katika uzima wa milele. Arusi ya Ndoa yetu na Kristu inaanza na Ubatizo inaendelea kila siku kwa Njia ya Ekaristi na itakamilika katika uzima wa mbinguni.

Tufurahi na kushangilia, tumtukuze kwani wakati wa Harusi ya Mwana Kondoo umefika na Bibi arusi yuko tayari…heri wale walioalikwa kwenye harusi ya Mwanakondoo“(Ufu 19:6-9).

2.       Ukristu ni gharama

Maana Ufalme wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu”(Rum 14:17).

Hapa Paulo hapingani na tulivyosema kuwa ‘Ukristu ni furaha’ bali anatukumbusha ile furaha ya kweli inayotokana na kutenda mema na anatukumbusha kuwa tunahitaji juhudi endelevu kubaki katika Ufalme wa Mungu.

a)     Ukristu ni gharama kwa sababu Unadai kuachana na mambo ya dunia

Wale walioalikwa harusini walikataa wakaenda ‘mmoja shambani kwake, mmoja kwenye bishara yake na wengine wakawauwa watumwa.’ Hii inatuonyesha kuwa

  • Shughuli za kawaida za maisha zinaweza kutufanya tusiingie katika ufalme wa Mungu.
  • Hii inawezeka pale tunapohangaikia sana usalama wa mwili bila kushughulikia uhusiano wetu na Mungu.
  • Tunapotafuta pesa kwa njia yoyote ile hata kwa kuiba au kuwanyang’anya wengine, tunapotumia njia zisizo halali na zisizo za haki katika kujipatia mali.
  • Tunapotumia muda wote kutafuta maisha na tukashindwa kutenga muda wa sala. Too much preocupation with our life takes us away from God.We may struggle to make a living and fail to make life.
  • Kazi tufanye, pesa tutafute lakini kwa njia halali na kila mara tumshirikishe Mungu mipango yetu yote.

 

b)     Ukristu Unadai kuweka juhudi ili kubaki katika Ufalme wa Mungu

Yule aliyekutwa hana vazi la harusi alitolewa nje ya ukumbi. Kuingia katika ufalme wa Mungu haitoshi lazima tuweke juhudi kudumu katika ufalme huo. Mungu anatuita jinsi tulivyo ili atufanye jinsi alivyo.

 

Tunapokuwa Wakristu lazima kuwe na mabadiliko katika maisha yetu. Lazima tuvae vazi la harusi yaani usafi na tujitahidi kudumu hivyo kwa njia ya sala na sakramenti. Tusipofanya hivyo, mahitaji ya maisha na mateso tunayokumbana nayo yanaweza kutugeuza nia yetu. Paulo ametwambia “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Lazima kila mara tuwe tumeungana na Kristu kwa sala na sakramenti ili atutie nguvu na hivyo tudumu na vazi la harusi na kuzaa matunda na hivyo tutakuwa na FURAHA.

Login Required

Leave a Comment

You must be logged in to post a comment.

Quote of the Week
Quote  of the Week

"Je, Wanipenda?"

November 2019
M T W T F S S
« Oct    
 123
45678910
11121314151617
18192021222324
252627282930  
Find me on Facebook
Follow me on twiter